http://deloplen.com/afu.php?zoneid=2607779 MORO NDIO HOME: May 2019

Wednesday, May 8, 2019

PENDEZA NA T-SHIRT KALIIIIII ZA #morondiohome




                                 Baadhi ya Wachezaji wakiwa wametupia Tishet zao pendwa
Upande wa kushoto ni DOKTA ALFRED MAPUNDA,MWALIMU NDEVU NA ADMIN DULLAH



                     Admin Dullah akiwa na Mtangazaji wa EFM RADIO wakuitwa Asha Manga
                           
                                                 Dokta Alfred akiwa na Familia yake
                                                     

                                              Admin Dullah akiwa na Mwalimu Ndevu
                                                   
                                          Homeboy Brigante Mo akiwa ametupia Tshirt yake BLACK
                                         

                                               Homeboy akiwa ametupia Kitu black

Monday, May 6, 2019

HISTORIA YA WATAWALA WA KILUGURU


WATAWALA WA JADI WA ULUGURU…

Tulikotoka:
AFRIKA ina makabila takriban 3,000 ambayo mamilioni ya Waafrika wanajinasibisha nayo kupata utambulisho; ni utambulisho ndiyo unaofanya wanajamii kujuana, kufahamiana, na kuyasukuma mbele maisha yao.
...
Makabila haya kila moja lina upekee katika Utamaduni na kwa ujumla ustaarabu na mifumo yake ya maisha, sanjari na taratibu za kiutawala. Waluguru ni moja kati ya Makabila hayo.

Takriban makabila yote ya Tanzania wakiwemo Waluguru yana utajiri mkubwa wa Historia na taratibu bora za kiutawala.

Waluguru wameishi kwenye safu ya Milima ya Uluguru kwa miaka mingi, japo wanahistoria wa kimamboleo wanarekodi kuwa, kati ya mwaka 1600 Dola tatu za Kiluguru, zilianza kuwa kwenye upeo wa juu wa ustawi wa kijamii, kiuchumi na kitamaduni chini ya serikali zenye taasisi imara na kamilifu.

Watawala wa mwanzo wa jamii hii ni pamoja na Mbago alieongoza himaya ya Wamwenda; Mtawala Magoma aliyeongoza utawala wa Tegetero, na Hega akiongoza Utawala wa Uluguru kusini (akiwa na makao yake Bwakila Juu, utawala wake ukitandawaa hadi kwenye baadhi ya maeneo ya Wakutu).

Lakini pia zipo simulizi na baadhi ya tafiti zenye mashiko kuwa, Mtawala wa mwanzo wa Kiluguru ni Mbago aliyeanza kwanza kuishi na jamii yake katika maeneo ya tambalare kusini ya Uluguru (yaani kwenye eneo linalofahamika hivi leo kama hifadhi ya Selous, kabla ya kuja Mtawala Hega na jamii yake na kwa pamoja wakatamalaki kwenye milima ya Uluguru; na kiongozi wa wa tatu kuja eneo hilo ni Mtawala Magoma wa Tegetero, na kisha watawala wengine kama kina Msumi (aliyetawala Kibungo Juu), Bambalawe (matombo) na aila zao akiwemo Mleke Mwanamsumi au kwa jina maarufu Kingalu Mwanamsumi (Kingalungalu) ama Kingalu wa kwanza aliyetawala eneo kubwa la Uluguru kuanzia Kinole (milimani mpaka wa kusini wa Dola yake yalipo makao makuu yake) hadi Ukami (Tambalale iliyotandawaaa sehemu ya Mikese upande wa Magharibi, sehemu ya Turiani Kaskazini, sehemu fulani ya Pwani hadi sehemu fulani ya Mzizima (yaani kusini Magharibi ya Dar es Salaam).

Na kati ya mwaka 1680 hadi 1850 pakaongezeka tawala nyingine yaani ya Mtawala Mdeng’o wa Magadu (kuanzia eneo la SUA la sasa, Magadu, Luhungo, Mkoya, Mzinga, Kauzeni, Tangeni, Konga, Mindu, Madaganya, Mzumbe, Changarawe, hadi Mlali).

Pia utawala wa Lukwele Mwanamzeru wa Dola ya Choma yaani sehemu ya Morogoro Kusini Magharibi Nyiachiro) na milima inayotazama Manispaa na tambarare yake hadi sehemu ya Kaskazini Magharibi na Magharibi ya wilaya ya Mvomero ya sasa (aliyetawala mwaka 1850 hadi 1865) akirithiwa na mpwawe Lukwele Mdimang’ombe Mwanamsumi II (mwaka 1865 hadi 1971).

Na baada ya vita ya kwanza ya Dunia hususan mwaka 1918 pakaasisiwa tawala mpya ya Ulelengwe iliyomegwa toka kwa wamwenda ikijumuisha maeneo ya tambarare ya kaskazini Magharibi ya Uluguru (Sangasanga, Merela, Doma, Mangae, Msongozi, Magali, Mtipure, Mkata, pembezoni mwa hifadhi ya Mikumi na maeneo mengine ya jirani).

Kwa upande mwingine, pembezoni mwa Uluguru yaani Turiani alikuwepo mtawala wa Kizigua aliyeitwa Kisebengo, ambaye alihamia kwenye Tambarare ya Uluguru na kubatizwa na watawala wa Kiluguru lakabu ya ‘Kingo’ (baadaye kizazi chake kiliasisi mji wa Simbamweni na kisha sehemu fulani ya mji wa sasa wa Morogoro na eneo la Kingoluwila kwa mtawala).

Sayyid Sultan Kingo Kisebengo alitawazwa na sayyid Salum Lukwele Mdimang’ombe (lukwele II) wakati huo akiwa ‘Gungulugwa’ (Crown Prince) wa Choma, kwa maelekezo ya Baraza la Falme za Kiluguru kuwa Sultan wa kwanza wa Morogoro.

Tunamtaja Sultan Kisebengo (mashuhuri kwa lakabu ya ‘Kingo’) kwa kuwa aliacha alama kwenye maendeleo ya Uluguru na kuasisi mji wa Morogoro; lakini pia kwa kusaidia sio tu ulinzi wa Kaskazini ya eneo la Dola Tisa ndogondogo za Kiluguru, bali pia kudhibiti usalama wa watumiaji wa barabara kuu ya kwenda bara kwa upande wa kaskazini ya Milima ya Uluguru dhidi ya maharamia, na kusaidia kukusanya mapato kwa niaba ya Watawala wa Uluguru kwa watumiaji wa barabara hiyo ya Kimataifa wakati huo (ambayo yalitumika kugharamia ulinzi na usalama wao na mali zao).

Vyeo vya Serikali za Machifu wa Kiluguru:
Hadi karne ya 20 Uluguru ilishatawaliwa na idadi kubwa ya Wafalme (Masultani au Machifu); lakini pia kulikuwa na wasaidizi wa Wafalme wakiwa na majina na majukumu tofauti.

Wandewa (Sub Chiefs):
Kundi la kwanza la wasaidizi wa Wafalme wa Kiluguru ni lile la ‘Wandewa’ au ‘Machifu wadogo’ (Waingereza waliwaita ‘Sub Chiefs’. Hawa walikuwa na mamlaka ya kifalem ya utawala wakiwa na vyombo vyao vya ushauri na usaidizi; wakishughulika pia na masuala ya ulinzi na usalama wa ndani, uchumi, utamaduni, mazingira, na huduma zote za kijamii, lakini hawakuwa na mamlaka ya mambo ya nje au Ulinzi wa nje (yaani kuwa na mamlaka ya majeshi ya vita), japo walipewa mamlaka ya Uhamiaji kwa ridhaa ya Sultani (Paramount Chief au Mfalme).

Waliokuwa mashuhuri ni kama vile kina Mndewa Fuko wa Kinole chini ya Utawala wa Kingalu Mwanafuko, Lugege aliyekuwa Mzinga chini ya Utawala wa Magadu; Mndewa Magona aliyekuwa Kisaki akiwaongoza Wakutu (bosi wake akiwa Sayyid Hega wa Uluguru Kusini); Mndewa Mtitu Mlapakolo aliyekuwa chini ya utawala wa Choma akiongoza eneo la Ruvuma (Morning side); Mndewa Mdede aliyekuwa chini ya utawala wa Choma akiongoza eneo la tambarare la Uluguru; Mndewa Nzota aliyeongoza Maeneo yanayofahamika hivi leo kama Forest Hill hadi eneo la sasa la Mkuu wa wilaya (Chini ya Dola ya Choma); Mndewa Betelo aliyeongoza eneo linaloitwa Bungo Dimwe (kuanzia shule ya Bungo karibu na chuo cha ardhi hivi sasa hadi Bungo Milimani chini ya Dola ya Choma); na Mndewa Msigala aliyetawala Chikangaga (kwa sasa panaitwa Lugala) chini ya dola ya Choma.

Mwingine mashuhuri zaidi ni Mwande “akifahamika kama mwenye nchi” (‘Mwenye Insi’ au ‘Mwenye Isi’) aliyekuwa mtawala wa Kibwe chini ya Dola ya Choma, lakini pia ndiyo Mkuu wa Wandewa wote wa Choma, hata Lukwele wa II Mdimang’ombe kabla ya kuwa Sultan alilelewa na kutumwa kazi na ‘Mndewa Mkulu’ Mwande ambaye kwa upande wa pili ni shemeji yake, yeye Lukwele akiwa Gungulugwa (Crown Prince) na Mndewa wa Choma (yaani maeneo ya sasa yanayoanzia kwa Mkuu wa Mkoa hadi juu milimani);

Waharatwaga (Regents):
Pia katika wasaidizi wa Wafalme wa Kiluguru kulikuwa na ‘Waharatwaga’ au ‘Wanaotawala jina’; hawa wanaweza kuwa katika eneo la Uchifu na hata Undewa (Waingereza wakiwaita ‘Regents’).

Kazi ya ‘Muharatwaga’ ni kutawala kwenye eneo ambalo Chifu au Mndewa bado hajapatikana, au amepatikana ila umri wa kutawazwa bado haujafika (yaani bado mtoto).

Pia Muharatwaga huweza kuongoza timu ya baraza tawala kwenye kipindi cha mpito baina ya utawala uliopita na ujao (Interregnum).

Maeneo ya aina hiyo yanayoongozwa kimpito ni pamoja na kwa ‘Walelengwe’ ambapo Ukoo wa Msimbe unadhibiti nafasi ya ‘Uharatwaga’, na Magadu ambapo Ukoo wa Mdeng’o unashika jukumu hilo kwa sasa.

Pia hali nyingine inayoruhusu uwepo wa Muharatwaga ni pale yeye mwenyewe (Muharatwaga) akiwa amepitishwa tayari kuwa Chifu Mkuu (Paramount Chief) na kutawazwa na Ukoo pamoja na Machifu wenzake chini ya usimamizi wa ‘Wahunga’ (Wanasheria za jadi) na ‘Waghongo’ (Watani), lakini lakini bado hajamaliza kutawazwa mbele ya wananchi wake yaani anakuwa ‘Chifu Mteule’, kama ilivyo sasa kwa eneo la Choma, ambapo ‘Muharatwaga’ Mussa Bwakila Lukwele amepitishwa hatua zote na kwa ukamilifu ameshakuwa ‘Chifu Lukwele wa IV’, na ameshaanza kufanya kazi kama ‘Mtawala wa Choma’ kwa upande mmoja, na Katibu wa Baraza Kongwe la Jadi la Machifu wa Uluguru chini ya Uwenyekiti wa Chifu Kingalu Mwanabanzi wa 15 kwa upande wa pili, lakini hajatawazwa kwa mara ya tatu na ya mwisho (hadi hapo atakapopanga na kuamua mwenyewe ndani ya muda usiozidi miaka mitano).

Baadhi ya Waharatwaga waliokuwa mashuhuri ni ndugu watatu wa Segumba walioishi eneo la Madizini kata ya Kilakala Morogoro mjini, ambao kwa vipindi tofauti vya miaka 30 waliongoza jopo lililosimamia na kutawala Choma baada ya kifo cha Lukwele wa II (kuanzia mwaka 1971).

Gungulugwa (Crown Prince):
Wasaidizi wengine wa Wafalme wa Kiluguru ni ‘Magungulugwa’ (Waingereza huwaita ‘Crown Prince’) yaani warithi wa Ufalme ambapo kwa tawala nyingi za Kiluguru wanashika nafasi ya tatu nyuma ya Manaibu Wafalme au Manaibu Chifu, na katika baadhi ya tawala wao huwa ndio Manaibu Chifu, ilhali kwenye tawala nyingine ‘Magungulugwa’ pia huwa ‘Mawaziri Viongozi’ (Chief Ministers).

Ikumbukwe kuwa, katika tawala za Kichifu Uluguruni tangu jadi, Baraza la Mawaziri huwa ni Dogo sana, pengine likiwa na mwaziri sita (pamoja na wasaidizi wao huwa jumla ya watu 12), isipokuwa kwenye utawala wa Kingalu yeye huwa na baraza kubwa kiasi la Mawaziri japo halina idadi ya kudumu (yaani idadi hubadilikabadilika kutegemea na wakati na aina ya mtawala, japo zipo wizara ambazo kijadi kamwe hazibadilishwi na ni lazima ziwepo).

Kati ya wengi, walio mashuhuri ni ‘Magungulugwa’ wa vipindi tofauti vya utawala wa Ukoo wa Kingalu, ambao mara kadhaa huishi mbali na makao makuu ya Chifu (yaani kwa Kingalu Gungulugwa na Chifu wanaishi mbalimbali na hata kazi za kila siku za Chifu wa sasa hufanywa na Naibu Chifu Mzee Kitiga kuliko Gungulugwa kwa mujibu wa mpangilio wao wa kimila wa utawala wa Sayyid Chifu Kingalu).

Mwingine ni Patric Kunambi aliyekuwa Gungulugwa wa Matombo na Naibu Sultan wa Morogoro toka ukoo wa Waingu chini ya Chifu Sabu Bin Sabu (Sultan wa Morogoro). Chifu Kunambi baadaye alikuja kuwa Sultan wa Morogoro baada ya kushika nafasi ya Mjomba wake Sabu Bin Sabu kiasha kuingia kwenye mawanda ya Kisiasa na hatimae kuzama kwenye ulimwengu wa wanataaluma akiwa kiongozi mwandamizi wa mwanzoni wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Mshenga (Head Man):
Aidha kuna Msaidizi mwingine muhimu ambae huitwa ‘Mshenga’ (Waingereza huwaita ‘Head Man’) ambae mara nyingi ni Mkuu wa koo, akiongoza zaidi ya kaya 500 chini ya utawala wa ‘Mndewa’, kawaida ‘Mndewa’ mmoja huwa na ‘Washenga’ wasiopungua wanne kutegemea idadi ya kaya, rasilimali fedha, na ukubwa wa eneo lake la utawala, wengine huzidi kumi), nao chini yao huwa na watu wanaoitwa “Viherehere” (Pioneers) ambao ni wasaidizi wakuu wa ‘Washenga’ (hivi leo wanafana kazi zao na Maafisa watendaji wa Mitaa japo kwenye kazi zao za jadi wanakwenda mbali Zaidi ya hapo).
Washenga hufanya kazi karibu zote za Mndewa katika ngazi ya eneo lake la Ushenga (kama walivyo Wenyeviti wa Mitaa hivi leo) isipokuwa masuala makubwa ya kinchi. Yeye ni kiunganishi baina ya Familia, Koo na Utawala wa juu yake (yaani Wandewa).

Mshenga mbali na kusimamia shughuli za kijamii, kiuchumi, mazingira na utamaduni, lakini pia yeye ndiye msingi wa kuleta furaha na Amani kwenye jamii, kwa kuwa anaongoza kwenye mizizi ya umma (yaani familia).

Ni yeye ndiye anayegawa daftari la familia na daftari la Ukoo kwa kila Ukoo na kila familia iliyo kwenye eneo lake la ushenga (Family Register and Clan Register); ni katika madaftari hayo ndimo kila mwanafamilia anayezaliwa husajiliwa na anayekufa pia huwekwa kwenye daftari ljeusi la wafu ambalo kila mwaka huwakumbuka kwa kuwasomea dua ya pamoja; na daftari la Ukoo ambalo kila mwanaukoo husajiliwa kwa kunakili madaftari ya familia yanayojenga ukoo husika. Nakala ya madaftari haya hukaa kwenye ofisi za Mshenga, na nakala hubaki kwenye familia na wakuu wa Koo husika (Clan Leaders).

Kazi nyingine muhimu sana ya Washenga wakisaidiana na “viherehere” ni kukutana na wakuu wa ukoo kuhakikisha kuwa koo na familia za kiluguru zinaishi kwa Amani, mapenzi, huruma, mshikamano, umoja na kwa ujumla kuimarisha udugu wa kweli; Kuhakikisha pia kuwa koo na familia za Kiluguru zinafuata sheria za nchi, miiko ya mila na desturi (yaani kukumbatia utamaduni wao mathalan wa kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana, kuimarisha taasisi ya ndoa, kutatua migogoro ya kiukoo na kifamilia, kuhakikisha kila mtoto wa ukoo anapata elimu na huduma zote muhimu za kijamii, na kuhakikisha kila mwanaukoo ana kazi halali ya kumuingizia kipato).

Jambo la mwisho na muhimu sana ambalo washenga husimamia, ni kuelekeza fursa za kiuchumi na ajira, sanjari na kuhakikisha kuwa kila ukoo unakuwa na “MFUKO WA UKOO WA MAENDELEO, SHEREHE NA MAZIKO”. Ni mifuko hiyo ya ngazi ya Ukoo ndiyo inayotoa usaidizi wa ada za shule, na mitaji ya biashara sanjari na matibabu kwa mwanaukoo mwenye hitajio, pamoja na kugharamia sherehe muhimu hasa za harusi, kugharamia maziko, na gharama za vikao vya ukoo husika. Wanaukoo huchangia “Nguto” (ada ya kijadi) kwenye mfuko huo ambao huwa ‘nguvu ya uchumi wao’. Mfuko pia unaweza kumiliki miradi ya maendeleo kwa manufaa ya ukoo.

Wahunga (Traditionalists):
Pia kuna wasimamizi wa Mila na hata tiba ambao pia husimama kama Wanasheria wa Kiluguru, hawa huitwa “Wahunga” ambao husimamia mambo yote ya kimila (Traditions and Customary Issues) na ya kisheria ya tawala za Kiluguru (Traditional Justice Systems) na ndio huongoza kazi ya kuwatawaza Machifu, kutatua migogoro, kusimamia ujenzi wa amani kwa niaba ya Chifu au Mndewa (Peace Building Initiatives), na mengineyo yanayorandana na hayo.

Kiongozi wao huitwa “Muhunga Mkulu” au “Muhunga Dikulu” (kutegemea na eneo yaani kutegemea na Kiluguru cha wapi kinatumika).

Ikumbukwe kuwa, kuja kwa Dini hasa Uislamu na Ukristo, kumezifanya tawala nyingi za Jadi za kiluguru kupunguza na pengine kuacha baadhi ya mambo yanayosigana na Dini zao. Wahunga wa tawala nyingi za Kiluguru hivi leo husimamia Mila zile tu zisizosigana na Misingi au Mizizi ya Dini ya Uislamu au ya Ukristo.

Waghongo (Ritualists):
Lakini Muhunga hawezi kufanya lolote bila ya kuwepo mtu mwingine anayeitwa ‘Mghongo’, huyu kwa kawaida ni Mtani toka Ukoo mwingine ambae husaidiana na ‘Wahunga’ kulitekeleza jambo la Ukoo wa Chifu, Mndewa, au Mshenga, iwe kumtawaza Chifu, Mndewa, au Mshenga; au iwe kushughulika na sherehe au misiba, tafakuri, tiba, maombi (kwa baadhi ya maeneo ya Uchifu na Undewa) na mengineyo yafananayo na hayo (Traditional Tribal Music, Prayers, Healing, Meditation, Celebration, Tribal Rituals etc.). Ni lazima ‘Mghongo’ awepo ndipo mambo yaende (Lakini kama nilivyoeleza hapo kabla, kwa baadhi ya Tawala za Kichifu muingiliano wa mafundisho ya Dini kuu mbili yaani Uislamu na Ukristo umedhibiti baadhi ya kazi za Kimila za Waghongo kwa kuzipunguza au na nyingine kuziondoa kabisa).

Katika muundo wa serikali za Kichifu, Mghongo huwa na nafasi muhimu kwenye mawanda ya kitamaduni na kisheria, na kiongozi wao huitwa ‘Mghongo Mkulu’.

Mgoli Mkulu / Sultana / Malkia (The Queen):
Kwa upande wa wasaidizi wanawake, katika muundo wa tawala za Kichifu za Kiluguru kuna tofauti ya majina ya watu kutegemea na tawala au eneo; tawala nyingine zote za Uluguru isipokuwa utawala wa Choma, Malkia au mke wa Mfalme, Chifu, Mndewa, Mshenga, Kiherehere na hata Muhunga au Mghongo huitwa ‘Wagoli’ (ila wa Chifu na Naibu Chifu huitwa ‘Mgoli Mkulu’; ama kwa utawala wa Choma mke wa Chifu na Naibu Chifu huitwa Sultana, na wa viongozi waliobaki huitwa ‘Wagoli’, ila mke wa Mndewa Mkulu (Mkuu wa Wandewa) huitwa ‘Mgoli Mkulu’.

Kingalu Mwana-Fuko na hata Kingalu-Mwanakinoge; pamoja na utawala Sabu Bin Sabu na mrithi wake Partrick Kunambi walitumia Cheo cha “Sultana” kwa Malkia. (Ikumbukwe kuwa Machifu hao wanne wa Kiluguru waliwahi kutumia cheo cha ‘Sultan wa Morogoro’ (yaani Kiongozi au Mwenyekiti wa Machifu Wakuu wa Morogoro).

Malkia/Mgoli Mkulu/Sultana ndiyo Kiongozi Mkuu wa wanawake wote kwenye eneo la Uchifu Uluguruni, vinyo hivyo Wagoli nao huongoza wanawake wa maeneo ya utawala ya waume zao. Huwa na majukumu maalum ya kufanya katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya jamii. Majukumu hutofautiana baina ya tawala na tawala, kutegemea mila na desturi zao, ujuzi, uzowefu na mara chache matakwa ya wahusika.

Kwenye baadhi ya tawala za Kichifu za Kiluguru Mke wa Chifu, au kama yuko hai Mama yake Chifu, au Bibi yake wakiitwa ‘Mama Malkia’ (Quean Dowager), husimamia ndoa za wanafamilia wote wa kichifu akiwemo Chifu mwenyewe (hata akitaka kuongeza mke wa pili au Zaidi ofisi ya Malkia au ya Mama Malkia hufanya kazi hiyo).

Na huku nyuma, takriban miaka 100 tu iliyopita, Ofisi ya Mama Malkia (Queen Dowager) pia ilihusishwa na mchakato wa kupata Mfalme / Sultan / Chifu mpya na hata Mndewa! Na ilikuwa na turufu (Veto) katika mchakato huo!

Miongoni mwa Masultana maarufu ni Sayyida Sultana Bernadeta Kunambi mke (Queen Consort) wa Sayyid Patrick Kunambi Chifu wa matombo na Sultan wa Morogoro; Sayyidat Sultana Tamasha Bint Abdallah Mbilikila aliyekuwa mke wa mtawala wa Choma (Sultan Salum Lukwele II Mdimang’ombe Mwanamsumi) ambaye ni Mpwa wa Sultan Kingalu Mwana-Fuko.

Majina ya vyeo vya Kifalme Uluguruni:
Watawala wa Kiluguru walitumia majina ya vyeo kwa Kiluguru kutegemea enzi ya Kiukoo (Dynasty) hasa kuanzia miaka ya 1600 hadi mwishoni mwa 1700. Kwa mfano Kingalu hakutumia jina lingine lolote zaidi ya ‘Ukingalu’ wake, yaani mtawala wa kwanza akawa Kingalu wa kwanza, ikaendeleo hivyo hadi sasa wa 15, labda kinachobadilika ni Mtala (Lineage), Mathalani Kingalu ‘Mwanamsumi’ (Kingalu wa kwanza), hadi Kingalu ‘Mwanabanzi’ (Kingalu wa 14 na wa 15).

Kwa hivyo neno “Kingalu” (kifupi cha Kingalungalu) lilisimama badala ya neno “Mfalme” au “Sultan” au “Amiri” au “Chifu Mkuu” (Paramount Chief) au “Mtawala”; na hali kama hiyo pia ilikuwa kwa Mdeng’o wa Magadu na kwa Mbago wa Mgeta n.k.

Sultan:
Baadhi walioathiriwa na mazingira ya Pwani walitumia majina yenye asili ya Kiarabu (cheo cha ‘Sultan’ kuanzia miaka ya 1800 hadi 1918) hasa baada ya Umashuhuri wa jina hilo kuvuka mipaka ya Zanzibar, Mafia, Kilwa na Comoro, na kutandawaa kwenye dola za bara na kuingia ndani hadi Kongo (Mashariki ya DRC ya sasa)! Kwa mfano Mtawala wa Dola ya Choma yaani Lukwele Mwanamzeru wa kwanza (1850 hadi 1865), na Lukwele wa Pili yaani Salum Lukwele Mdimang’ombe Mwanamsumi (1865 hadi 1971), walitumia jina la Sultan japo neno “Lukwele” peke yake lilitosheleza kusimama badala ya “Sultan”.

Chifu Mkuu au “Chifu” (Paramount Chief or “Chief”):
Neno la Kiingereza ‘Chief’ au Waswahili wakitamka “Chifu”, lilianza kutumika rasmi Uluguruni kuwatambulisha Wafalme wake kwenye mawanda ya serikali ya Kikoloni ya Waingereza kuanzia miaka ya 1918 hadi 1962 (pale Wafalme wa jadi walipoondolewa kwenye utumishi wa serikali na nafasi zao kufutwa kwenye sheria mama yaani Katiba). Hata hivyo wakaendelea kutumia neno hilo la ‘Chief’ nje ya utumishi wa umma, yaani kuanzia mwaka 1962 hadi hivi leo sanjari na majina ya vyeo ya kikabila (ya kijadi).

Niwakumbushe tu kuwa, wakati wa Utawala wa Waingereza walitaka mtu mmoja tu ndiyo aitwe “Sultan yaani Mwenyekiti wa Baraza la Watawala wa Uluguru. Hivyo watawala waliobaki ambao ni Wajumbe wa Baraza hilo waitwe Machifu (Chiefs).

Katika hilo, viongozi wa mwisho kuitwa hivyo chini ya utawala wa Waingereza, ni ‘Sultan’ Sabu Bin Sabu na mpwa wake ‘Sultan’ Patrick Kunambi (Tafuta asili ya kata ya “Sultan Area” mjini Morogoro kupewa jina hilo).

Hitimisho:
Chini ya utawala wa Ujerumani na baadaye Utawala wa Kikoloni wa Uingereza, Dola za Kiluguru zilinyang’anywa ‘mamlaka’ japo zilibakiziwa ‘madaraka’ ya utawala usio wa moja kwa moja (Waingereza wakiita ‘Indirect Rule’), ikiwa ni sehemu ya mipango ya muda mrefu ya Mataifa ya Magharibi, sio tu kuitawala kikamilifu Afrika bali pia kupora mali zake na kuvuruga Utamaduni wake, Maendeleo yake, na kwa ujumla Ustaarabu wake.

Image may contain: 2 people, people smiling, people standing and text

JE UNAIJUA HISTORIA YA IKULU YA MOROGORO???

PALE IKULU YA MOROGORO ILIPOGEUZWA HOSPITALI YA JESHI….

JE WAJUWA? Ni katika vita ya kwanza ya Dunia baina ya Ujerumani na Uingereza kuanzia mwaka 1914 hadi 1918, Boma au Ikulu ya Morogoro ilitumiwa kuwa Hospitali ya majeshi ya Ufalme wa Uingereza, wakati huo kwenye ukanda huu majeshi hayo yaliongozwa na Jenerali Smuts.

(Morogoro Boma had been used by the British as a hospital in the 1914-18 First World War between Great Britain and Germany; the British Empire troops in East Africa were commanded by General Smuts.)



Image may contain: sky, plant and outdoor